Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Msichana wa umri wa miaka kumi na saba wa shule ya St Jude Seregeya aliyejitia kitanzi siku ya Jumatatu atazikwa nyumbani kwao eneo la Soy hapo Kesho, Jumamosi.

Mwanafunzi huyo, Joyce Wanjiru, anaripotiwa kujitia kitanzi baada ya mwalimu mmoja kutoka shuleni humo kumnyang'anya simu ya rununu aliyokuwa nayo siku hiyo ya Jumatatu.

Joyce anasemekana kwenda shuleni mapema Jumatatu ili kuchukua karatasi za mitihani za marudio kabla ya simu iliyokuwa mfukonio mwake kuanguka na kuchukuliwa na mwalimu ambaye alimtuma kwenda kumleta mzazi wake kwa kuwa simu za rununu ni marufuku kwa wanafunzi shuleni humo.

Ni kisa hiki ambacho kilipelekea kujitia kitanzi kwa msichana huyo wa kidato cha tatu ambaye kulingana na majirani huenda alititoa uhai kwa kuhofia hasira za babake mzazi.

Naibu wa chifu wa eneo hilo Diana Owano, aliyethibitisha kisa hicho, aidha amewataka wazazi kutowakaripia na kuwachapa wanao kila wakati, akisema kuwa kuna mbinu ya mazungumzo ambayo pia hufanya kazi.

Kufuatia hicho, Owano ametoa wito kwa walimu, wanafunzi, wazazi na jamii kwa jumla kujukumika ili kuona kuwa kizazi kinachokuzwa kinakuwa na maadili, huku akiwataka wazazi kuwaelewa watoto wao ambao ndio kwanza wanakuwa na kusema kuwa changamoto wanazozipitia ni nyingi mno.