Mwanamke mmoja amehukumiwa mwaka gerezani kwa madai ya kumvamia jirani yake na kumjeruhi katika eneo la Kinoo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mary Wanjira alifikishwa mbele ya Hakimu mkuu James Ogweno siku ya Ijumaa katika mahakama ya Kikuyu.

Kiongozi wa mashtaka aliwaleta mashaidi watatu ambao walitoa ushaidi wao.

Mshaidi wa kwanza, Grace Nyawira ambaye ni jirani ya wawili hao alisema kwamba mnamo Juni 2, 2015, mshukiwa ambaye alikuwa nyumbani kwake alianza kuongea kwa sauti ya juu akimkashifu mlalamishi Nancy Wairimu kwa madai kwamba alikuwa anamyemelea mumewe.

Hata hivyo Bi Wairimu alitoka nje na kumwita mshukiwa na kumuuliza kwanini alikuwa akimtusi.

Mshukiwa alizidi kumtusi na kumwaribia jina miongoni mwa majirani wengine akimwita mwizi wa wanaume wa wenyewe.

Mshaidi alieleza kwamba Wanjira alimvamia Wairimu na kumpiga akitumia fimbo na kuwalazimu majirani kuiingilia kati na kukatiza kisa hicho.

Hata hivyo, Wairimu alikuwa amepata majeraha na wakampeleka hospitalini.

Mshaidi wa pili, Bwana Richard Otieno, ambaye ni daktari katika hospitali ya kibinafsi ya Shallon katika eneo la Kinoo, alisema kwamba Wairimu alipelekwa hospitalini akiwa anavuja damu akiwa amebebwa na wanawake wanne.

Allisema kuwa alimfanyia Wairimu operesheni ndogo kwani alikuwa ameumia kichwani, na pia alipoteza jino mmoja pamoja na kupata majeraha mengine madogo mguuni, mkononi na mgongoni.

Mshaidi wa tatu, Afisa wa polisi aliyekuwa anachunguza kesi hiyo, Sergent Ali Mohamed kutoka kituo cha Polisi cha Kinoo, alisema kwamba Wairimu alienda kurepoti kisa cha kuvamiwa na jirani yake kwa madai kwamba alikuwa na uhusiano na mume wake.

Mohamed alidhibitisha kwamba alikuwa mchunguzi wa kesi hiyo na waliandamana na askari wawili mpaka pale ambapo walikuwa wakiishi na kumtia Wanjira mbaroni.

Mohamed alidhibitisha kwamba fomu ya P3 iliandikwa na daktari na kudhibitisha kwamba mlalamishi aliumizwa.

Hakimu Ogweno katika hukumu yake alimhukumu mwaka mmoja gerezani bila faini.