Mwanamke mmoja ametozwa faini ya Sh30,000 na mahakama moja ya Nakuru baada ya kupatikana na kosa la kuendesha biashara ya uuzaji wa pombe haramu.
Sarah Chepsang alishikwa na maafisa wa usalama Jumanne wiki iliopita akiwa na lita 15 za pombe inayojulikana kama kangara katika eneo la Solai lililoko Rongai katika Kaunti ya Nakuru.
Kwa mujibu wa polisi, Chepsang alikuwa amekamatwa kufuatia operesheni ya kukabiliana na pombe haramu katika eneo hilo iliyotekelezwa na maafisa wa usalama wa eneo la Njoro waliompata bila leseni ya mwaka huu inayomruhusu kuendesha biashara hiyo.
Alipofikishwa kizimbani mbele ya Hakimu Liz Gichae, Chepsang aliyakubali mashtaka hayo na kuiomba mahakama hiyo imsamehe na kumuachilia huru kwani biashara hiyo ndiyo aliyeitegemea kwa mapato yake ya kila siku.
Alisema kuwa alikuwa akifanya biashara hiyo kwani ndio ilikuwa njia pekee ya kukimu jamii yake na akaiomba mahakama imsamehe kwani yeye ndiye pekee alikuwa anategemewa na familia yake.
"Niliuza pombe hiyo ili kupata mapato ya kukimu jamii yangu, sina njia nyingine yeyote ya kujikimu na hivyo naomba mahakama hii inisamehe kwa kosa hilo," alisema Chepsang.
Licha ya ombi la Chepsang, mahakama hiyo ilimpata na hatia na hivyo ikampa adhabu ya faini ya Sh30,000 ama afungwe kwa miezi mitatu.