Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwanamke mmoja ametiwa mbaroni na maafisa wa polisi mjini Nyamira kwa madai ya kupatikana akisambaza karatasi za mtihani wa kitaifa wa KCSE unaoendelea kote nchini.

Akithibitisha kisa hicho siku ya Alhamisi, Kamanda mshirikishi wa maafisa wa polisi Kaunti ya Nyamira Kalimbo Mwandoe alisema kuwa mwanamke huyo, Marion Moraa, mwenye umri wa miaka 23, alitiwa mbaroni kwenye Shule ya mseto ya upili ya Ntana siku ya Jumatano mwendo wa saa tatu usiku akiwa na karatasi za somo la Historia, Hisabati, kiswahili, Biashara na lile la CRE.

"Maafisa wa polisi walitia mbaroni mwanamke huyo kwenye shule ya upili ya Ntana kwa kupatikana na karatasi kadhaa za mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne," alisema Mwandoe.

Afisa huyo wa polisi alisema kuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo Dalmas Arwa aliwaarifu maafisa wa polisi waliofanikiwa kumtia mbaroni mshukiwa huyo huku washukiwa wenzake wawili wakifanikiwa kutoweka kwa kwa kuruka ua wa shule hiyo.

"Mwalimu mkuu wa shule hiyo ndiye aliye waarifu maafisa wa polisi kuhusiana na swala hilo na papo ndipo walipochukua hatua na kumtia mbaroni mshukiwa huyo huku wenzake wawili wakifanikiwa kutoweka," alisema Mwandoe.

Mwandoe alisema kuwa maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi ili kuwatia mbaroni washukiwa waliotoroka.

"Tayari polisi wameanzisha uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na msako mkali wakuwasaka washukiwa hao wengine wawili waliotoweka umeanzishwa," alisema Mwandoe.