Mwanamke mmoja alimfumania mumuwe mwenye umri wa miaka 36 na mwanamke wa miaka 60 siku ya Jumatatu iliyopita wakijivinjari kwenye baa moja mjini Nyamira.
Mke huyo alidai kuwa mumewe anayefanya kazi ya kuuza na kutengeneza simu mjini humo amekuwa akimpelekea mwanamke huyo pesa zote huku watoto wao watatu wakiendelea kutaabika kwa njaa.
"Mume wangu alitoweka nyumbani wiki moja iliyopita na nimekuwa nikimtafuta bila mafanikio lakini hii leo, nimegundua kuwa ana mwanamke mwingine na pesa zote humpelekea yeye huku watoto wetu watatu mmoja wa kidato cha kwanza, darasa la sita na la tatu wakilala njaa,” alisema mwanamke huyo aliyetaka jina lake libanwe kwa sababu ya usalama.
Hali hiyo iliwapelekea baadhi ya wanawake wenye hamaki kuingilia kati ili kumsaidia mwanamke mwenzao kumtoa mumuwe kutoka mikononi mwa mwanamke huyo lakini juhudi zao zikaambulia patupu pale ambapo mwenye baa aliwafukuza huku wawili hao wakijifungia humo ndani.
Wanawake hao wamewataka wanaume kuwajibika hata kama wanapendelea 'mipango ya kando' kuliko wake zao.
"Hatujafurahishwa na jinsi 'mipango ya kando' inaendelea kuharibu ndoa nyingi lakini itakuwa vyema iwapo wanaume watawajibika kwa kuzilinda familia zao iwapo wameonelea kuwa ni lazima wawe na wanawake huko kando," walisema wanawake hao.