Mwanamume anayedaiwa kujaribu kujitoa uhai kwa kujipiga risasi mguuni alifikishwa kwenye mahakama moja ya Nakuru siku ya Jumatano kujibu shtaka hilo.
Mahakama ilielezwa kuwa mshtakiwa, Thomas Mugendi, ambaye pia alikuwa anatumia jina Mohamed Ali, alijipiga risasi kwenye mguu wake wa kushoto baada ya kumnyang’anya Simion Njeru ambaye ni afisa wa polisi, bunduki yake tarehe Oktoba 18 katika eneo la St Monica section 58 viungani mwa mji wa Nakuru.
Hata hivyo, upande wa mashtaka uliomba Hakimu mkuu Liz Gicheha kuamuru mshtakiwa awekwe rumande kwa siku tatu zaidi na kufanyiwa uchunguzi wa kiakili katika hospitali ya mkoa wa bonde la ufa iliyo Nakuru ili kubainisha iwapo anaweza kujibu shtaka hilo.
Wakili wa mshtakiwa aliomba hakimu mkuu huyo kuamuru mshukiwa afikishwe hospitalini akidai yuko kwenye hali mbaya kiafya kutokana na risasi iliyo kwenye mguu wake wa kushoto, akiongeza kuwa mshukiwa pia anahitaji kufanyiwa upasuaji ili kutoa risasi hiyo.
Kwa upande wake, Gicheha aliamuru mshtakiwa kusalia rumande katika Kituo cha polisi cha Nakuru na pia kufikishwa katika Hospitali ya bonde la ufa iliyo Nakuru kwa matibabu na uchunguzi wa kiakili.
Kesi hiyo itatajwa tarehe Oktoba 28, 2015.