Mwanamume mmoja wa miaka 38 alipatikana ameuawa akiwa na majeraha ya kichwa na mwili wake kutupwa kando ya barabara katika eneo la Mongoya, Kata ya Bomariba iliyoko eneo bunge la Bochari, Kaunti ya Kisii.
Akithibitisha kisa hicho siku ya Jumatano, chifu wa Kata ya Bomariba Trubosah Orina alisema huenda marehemu alishambuliwa na wajambazi ambao alisema hawajapatikana hadi sasa.
Wakati uo huo, chifu wa Kata ya Bogita aliyefika eneo la kisa hicho alisema mbinu itatafutwa ya kuimarisha usalama katika eneo hilo kwani visa vya mauaji vimeongezeka kila wakati katika eneo hilo.
Inasemekana kuwa marehemu alikuwa anatoka eneo la Kiango, lakini haijabanika waliomuua na kumuacha na majeraha makali kichwani.
Maafisa wa polisi kutoka Kituo cha Gesonso na wa Kituo cha Riana walifika na kuchukua mwili wa marehemu hadi chumba cha kuhifadhi maiti ya Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii huku uchunguzi ukiendelea.
Machifu hao wawili waliwaonya wakazi dhidi ya kunywa pombe na kutembea muda wa usiku wakiongeza ni kinyume.