Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwanamume wa umri wa miaka 20 katika kijiji cha Mokomoni, Wilayani Nyamira ametiwa mbaroni na maafisa wa Polisi wa Kituo cha Nyamira kwa madai ya kulawiti watoto watatu wa kiume.

Akithibitisha kisa hicho, mkuu wa polisi katika Kaunti ya Nyamira Ricah Ongare alisema mshukiwa huyo yupo chini ya ulinzi wa polisi katika Kituo cha Polisi cha Nyamira huklu akisubiri kufikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya vitendo hivyo vya aibu.

Akiongea na Waandishi wa habari mnamo siku ya Alhamisi, Mkurugenzi Mkuu katika Hospitali ya Nyamira Level Five Cyrus Ayunga alisema wavulana hao watatu wanaodaiwa kulawitiwa na mshukiwa huyo tayari wamekabidhiwa madawa ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.

Ayunga alidokeza kuwa wawili kati ya wavulana hao walifikishwa katika hospiatali kabla ya siku tatu tangu siku ya kudaiwa kufanyiwa unyama huo huku mwingine akifikishwa hospitalini baada ya wiki moja kukamilika.

Vile vile, mshukiwa huyo pia inasemekana kuwa na virusi vya Ukimwi. Waathiriwa hao inasemekana kuwa na umri kati ya miaka saba na minane.

“Ni ukweli mshukiwa huyo alikuwa na virusi vya Ukimwi na tayari hawa watoto watatu tumewapa madawa ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo na tutawapima baada ya mwezi moja kukamilika ili tuone jinsi walivyo kiafya,” alisema Ayunga, mkurugenzi katika hospitali ya Nyamira.