Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanasiasa aliyewania kiti cha eneo Bunge la Bochari katika Kaunti ya Kisii Voctor Omanwa amewaomba wakazi wa kaunti hiyo kutoandamana wanapotofautiana kimawazo ila kufuata njia iliyo bora ya kutafuta suluhu.

Hii ni baada ya wafanyikazi 300 wa Kaunti ya Kisii ambao hawakuwa wamelipwa mshahara kwa miezi 10 mfululizo tangu waajirwe katika kaunti hiyo kuandamana katika mji wa Kisii mnamo siku ya Jumatano wiki jana kulalamikia kutolipwa kwa mishahara yao.

Akizungumza mnamo siku ya Jumanne katika eneo la Tabaka, mwanasiasa huyo alisema kuandamana si suluhu bali kutafuta mbinu ya kutatua malalmishi kwa maelewano.

“Nawaomba msiwe mnaandamana kila wakati jambo mbaya linapotokea maana ni kuharibu jina la kaunti yetu ambayo imejulikana vizuri nchini haswa katika sekta ya kilimo,” alisema Omanwa.

Wakati uo huo, mwanasiasa huyo aliwaomba viongonzi kutoka eneo hilo kufanya maendeleo na kuajibika kwa yale wanastahili kuwafanyia wananchi ili kuwaridhisha jinsi wanaohitaji kwani viongonzi walichaguliwa kufanya maendeleo.

Pia mwanasiasa Omanwa alipongeza serikali ya kaunti hiyo kwa hatua imepiga haswa katika sekta ya afya ambayo imeimarika kuliko sekta zingine huku akimwomba Gavana Ongwae kuendelea kufanya maendeleo kwa sekta zingine ili ifikapo mwaka wa 2017 ipate maendeleo ya pande zote yameshughulikiwa kikamilifu jambo ambalo litamuwezesha gavana huyo kuchaguliwa tena.