Kijana mmoja wa kuendesha bodaboda aliponea kifo baada ya lori moja la kubeba mizigo kukosa mwelekeo kabla ya kumgonga na kumjeruhi vibaya miguu yote miwili siku ya Jumamosi mjini Kisii.
Ajali hiyo ilitokea katika barabara ya St. Judy katikati ya mji wa Kisii ambapo lori lililokuwa likitoka upande wa barabara ya Hospitali ya Kisii Level Six kukosa mwelekeo hadi kwenye kituo hicho cha bodaboda na kuzigonga bodaboda zilizokuwa zimeegeshwa kabla ya kumgonga mhudumu huyo wa bodaboda aliyekuwa akisubiria abiria.
Mhudumu huyo alirushwa hadi kugonga mti wa nguvu za umeme kabla ya kuanguka kwenye mtaro wa kupitisha maji.
Mhudumu mmoja wa bodaboda kwa majina Elkanah Mosiori, aliyeshuhudia kisa hicho, alimlaumu mwenye gari hilo kwa kutowajibika akisema lori hilo lilikuwa na nafasi kubwa ya kupitia badala ya kuja eneo hilo ambalo mara nyingi hutumiwa na bodaboda kama kituo cha kusubiria abiria.
Ghadhabu za waendeshaji bodaboda hao zilipanda baada ya dereva wa lori hilo kujaribu kutoroka ambapo walilipiga mawe lori hilo na kutaka kulichoma wasingekatazwa na mmoja wa viongozi wa steji hiyo Ken Mokaya.
Bwana Mokaya aliomba serikali ya Kaunti ya Kisii kuhakikisha kuwa magari makubwa, hasa ya kubeba mizigo yanazuiliwa kupitia njia hiyo kwani kisa kama hicho ni cha tatu mwaka huu mtu kugongwa akiwa amaegesha bodaboda na magari hayo.
Mjeruhi alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii Level Six huku lori hilo kupururwa hadi Kituo cha Polisi cha Kisii Central.