Wakaazi wa eneo la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu waliamkia kisa cha kushangaza walipopata mwili wa mwanamume mmoja anayedaiwa kuwa mwendeshaji bodaboda akiwa amefariki.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akidhibitisha kisa hiki siku ya Jumatano, Mkuu wa Polisi wa eneo la Kikuyu, Mutune Maweu alisema kuwa marehemu alikuwa mwendeshaji wa bodaboda katika eneo hilo na anadaiwa kuuwawa na watu wasiojulikana.

Alieleza kwamba mwili wa marehemu ulikuwa na alama za kukatwa na inashukiwa kuwa aliuawa kwa kukatwa katwa mara kadhaa.

Mkuu wa polisi alieleza kwamba waliotekeleza unyama huo walitoweka na pikipiki ya marehemu pamoja na simu na pesa.

"Waliotekeleza uuaji huo wanadaiwa kuwa majambazi ambao walijaribu kumwibia marehemu na katika shughuli hiyo, marehemu alijaribu kupimana nao nguvu kabla ya wao kutekeleza uuaji huo na kumwibia," alisema Maweu.

Maweu alieleza kwamba mwili wa marehemu utapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha city na uchunguzi umeanza kufuatia tukio hilo. 

"Uchunguzi umeanza kufuatua kisa hiki na tunafanya juhudi zote ili tuweze kudhibitisha waliotekeleza uovu huo. Tunawahakikishia waendeshaji bodaboda na wakaazi wote usalama wao na wasiwe na hofu kufuatia kisa hiki kwa kuwa tunafanya tuwezalo kuwatia mbaroni majambazi hao," alisema Maweu.

Erastus Njuguna, mwendeshaji bodaboda katika eneo la kikuyu alisema kwamba usalama ulikuwa umezorota hasaa wakati wa usiku.

Alieleza kwamba hali hii ilikuwa inawalazimu kufunga kazi nyakati za usiku kwa kuhofia maisha yao. 

Bwana Njuguna alihuzunika kwa kifo cha mwenzao akisema kwamba kifo hicho kimewapa hofu katika biashara yao.

Aliomba idara ya polisi kushika doria ili kuweza kuwahakikishia usalama.