Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mtu mmoja aliaga dunia kwenye ajali ya barabarani iliyohusisha lori mbili na pikipiki katika mzunguko wa Gate House mjini Nakuru.

Ajali hiyo iliyotendeka siku ya Jumanne, mwendo wa saa kumi na moja unusu jioni ilitokea wakati ambapo mmoja wa madereva hao wa lori alipojaribu kuingia kwenye mzunguko huo na hapo akamgonga mwendeshaji huyo wa pikipiki kutoka nyuma na kupelekea lori hilo pia kuligonga lori lingine kwa nyuma.

Mwendeshaji huyo wa pikipiki aliaga dunia papo hapo na kulingana na mmoja wa walioshuhudia ajali hiyo, misongamano inayoshuhudiwa katika eneo hilo nyakati za jioni iliongezeka baada ya ajali hiyo kutokea.

Dereva wa lori hilo alijeruhiwa na kupelekwa katika hospitali kuu ya mkoa iliyo mjini Nakuru.

Ajali hiyo iliyosababisha msongamano mkubwa wa magari ilipelekea maafisa wa polisi kuwaagiza wenye magari kupitia njia mbadala huku wakijibidiisha kuondoa magari hayo kwenye eneo la tukio.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika ufuo wa serikali ya Kaunti ya Nakuru huku lori hizo mbili na pikipiki hiyo zikibururwa hadi katika kituo cha polisi cha Central mjini Nakuru.