Mwenyekiti wa kandanda wilayani Marani, kaunti ya Kisii James Isaboke ameiomba serikali ya kaunti hiyo kukarabati uwanja wa michezo ulioko wilayani humo.
Wito huo umetolewa baada ya uwanja huo kuharibika pakubwa, ilhali unatumiwa kila mwishoni mwa juma na vijana wa kandanda wakati wa vinyanganyiro mbalimbali ambavyo huandaliwa na wahisani wema pamoja na wanasiasa.
Kulingana na mwenyekiti huyo, uwanja huo umeharibika, na anahitaji uwanja kukarabatiwa katika hali ya kisasa jinsi serikali ya kaunti hiyo ilivyoahidi hapo awali.
Akizungumza na mwaandishi huyu siku ya Jumatano katika mji wa Marani, mahala uwanja huo ulioko, Isaboke aliomba serikali ya kaunti hiyo kuukarabati uwanja huo ili uendelee kutumiwa na vijana bila kukumbana na changamoto wanapocheza.
“Uwanja huo umekuwa ukiahidiwa kila mara kuwa utakarabatiwa kwa muda mrefu, jambo ambalo halijawahi zaa matunda hadi sasa na kuendelea kusalia kuwa katika hali ya hapo mbeleni
“Uwanja huu ndio uwanja wa kipekee ambao hutumiwa na shule pamoja na vijana wa kandanda. Naomba serikali ya kaunti itukarabatie uwanja huu maana ni wa wilaya ya Marani na kuna haja ya kukarabatiwa,” alisema Isaboke.