Kijana mmoja alichomwa na wakazi kutoka eneo la Menyinkwa, kijiji cha Nyaura, divisheni ya Kiogoro kufuatia madai ya wizi.
Naibu chifu wa kata ndogo ya Nyaura ambaye alithibitisha kisa hicho siku ya Jumanne, Bwana Yobes Mose, alisema mwizi huyo alipatana na mauti yake baada ya kujaribu kuiba katika kata ya Masongo, ambapo alikimbizwa na wakazi baada ya kijana wa boma hilo kupiga kamsa.
Mose alisema wezi hao walikuwa watatu na wawili waliweza kutorokea msituni kutumia pikipiki na wakazi kufanikiwa kumpata mmoja wao na kumpiga na baadaye kumchomea kando ya barabara kuu ya kutoka Kisii kuelekea Kilgoris.
Marehemu alitambuliwa kama Alfred Onkoba anayetoka katika eneo la Getare, Kaunti ya Kisii kulingana na maelezo yaliyopatikana kwenye kitambulisho chake.
Kwenye patashika hizo za wezi hao kutaka kuiba kijana wa boma hilo aliweza kupigwa jiwe na kuzimia ambapo alipelekwa hospitali na anaendelea kupata matibabu kwenye kituo kimoja cha afya mjini Kisii.
Hata hivyo, naibu chifu huyo alitoa wito kwa wakazi kujiepusha na kuchukua sheria mkononi na kuwajibikia sheria kwa kuripoti visa kama hivyo kwenye mamlaka husika hasa kwenye ofisi yake au kwenye kituo cha polisi kilichoko karibu.
Hiki ni kisa cha pili cha wizi kutendeka kwa muda wa siku tano baada ya gari aina ya Probox kuibiwa kutoka eneo hilo la Kiogoro.
Chifu Mose aliwashauri vijana kutoka eneo hilo kuachana na uhalifu na kufanya shughuli ambayo ni halali katika harakati za kupata riziki ya kila siku.
Mwili wa marehemu ulichukuliwa na maafisa wa polisi katika hifadhi ya wafu ya hospitali ya Kisii Level Six.