Share news tips with us here at Hivisasa

Mzozo wa shamba baina ya mwenye ardhi na mwenye shule moja ya kibinafsi umesababisha shule hiyo iliyoko katika sehemu ya Mwembe kuchomwa na anayedaiwa kuwa mmiliki wa kipande hicho cha ardhi.

Shule hiyo, King James Liberty School, ilishika moto jana, Jumapili usiku, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni mafuta ya aina ya petrol yaliyomwagwa na mmiliki shamba hilo.

Kulingana na mwenye shule hiyo Bwana Jared Bora, ambaye aliongea na mwandishi huyu, zogo lilizuka siku ya Alhamisi pale ambapo mwenye shamba hilo alipotaka shule hiyo ihamishwe kutoka mahali hapo kwa sababu za kuchochewa na ndugu za mmiliki shamba.

Bora aliongeza kusema kuwa ijapokuwa hakulinunua shamba hilo, alikuwa analipia kodi kwa vile alilikodisha na wakaelewana hadi akamjengea mwenye shamba nyumba ya kuishi ila kutoelewana kumeanza tu juzi.

Bora, ambaye pia ni mwalimu wa shule hiyo, aliwashtumu ndugu za mwenye shamba kwa kuleta fitina baina yao, kwa kile anachosema ni tamaa ya kutaka kuuza ili apate pesa huku akiwataka wakae ili wazungumze ili wapate suluhu ya kudumu.

Hata hivyo, shule hiyo iliweza kupata msaada kutoka kwa wazazi, wahisani pamoja na serikali ya kaunti ya Kisii na kuanza kujenga madarasa upya.

Hakuna kitu kilichoweza kuokolewa kutoka kwenye mkasa huo.