Nafuu ya chakula itapatikana kwa siku chache tu kwa wakulima wa mahindi katika maeneo kadhaa ya Kaunti ya Kisumu.
Hii ni baada ya baadhi ya wakulima hao kuanza kuvuna zao hilo ambalo halikufanya vizuri sana msimu huu kutokana na mvua nyingi iliyonyesha miezi michache iliyopita.
Katika Wadi za Kabonyo na Ugwe, mahindi yameshuka bei kutoka Sh100 hadi Sh50 kwa kila mkebe wa kilo mbili, bei ambayo wakulima wanasema kwamba haitashuka kupita hapo na pia haitadumu muda mrefu kabla ya kupanda tena maradufu.
Karen Anyango ni mkulima wa mahindi wa kiwango cha kadiri ambaye tayari anaendelea kutoa mahindi yake shambani, anayedokeza kwamba kuna dalili za bei ya mahindi kuendelea kupanda muda mfupi baada ya kipindi cha mavuno kumalizika kwa kuwa mazao hayakufanya vyema na hivyo kusababisha mavuno duni,'' alisema Anyango.
Mashamba mengi katika Kaunti ya Kisumu yako katika maeneo ya miinuko na mabonde, hali ambayo ilisababisha maji kujaa katika sehemu za mabonde na baadaye mahindi kukauka kabla hayajakomaa wakati kiangazi kilipozuka siku chache baada ya mvua kukoma.
Kwingineko, wakulima walilazimika kuvuna mahindi yao mapema kabla ya wakati kutokana na wizi ulioshuhudiwa mashambani mwao.
Hali hiyo inatokana na hali ya upungufu wa chakula katika jamii nyingi katika maeneo hayo.