Naibu chifu wa Mwamonari amewaonya wanaotumia pesa bandia ili kujifadi wao wenyewe kuwa wakifumaniwa watakabiliwa kisheria.
Hii ni baada ya wafanyibiashara katika eneo la Sombogo, Wadi ya Sensi, kupeleka malalamishi hayo kwa naibu chifu wa lokesheni hiyo ya Mwamonari Nelson Atandi, huku wakidai kuwa kuna baadhi ya watu ambao wanatumia pesa bandia kununua bidhaa mbalimbali kutoka duka zao.
Atandi alisema yeyote atakayefumaniwa akizitumia pesa badia atatiwa mbaroni, ashtakiwe kortini na kufunguliwa mashtaka ili kukabiliwa kisheria.
Akizungumza katika eneo hilo la Sombogo siku ya Jumatatu, Atandi aliwasihi walio na pesa hizo kutozitumia tena na kusema uchungunzi umeanzishwa kubaini wahuni hao.
Agizo hilo lilipokelewa vyema na kuwafurahisha wakazi na wafanyibiashara wa eneo hilo huku wakitarajia kuwa utumizi wa pesa hizo bandia utakoma.
“Mimi mwenyewe naunga mkono agizo hilo kuwa anayepatika akiwa na pesa badia ashtakiwe kwani ikifika jioni mwendo wa saa moja utapata mtu anakukabidhi pesa badia, na unapofika kwa nyumba ndio unagundua kuwa pesa hiyo haikuwa halali,” alisema Alice Ochako, mfanyibiashara.