Naibu wa Gavana wa Kaunti ya Nyamira Amos Nyaribo amewaomba wanasiasa kukomesha tabia ya kupiga siasa katika sherehe za mazishi na maombolezi.
Akizungumza mnamo siku ya Ijumaa katika hafla ya mazishi ya mzee Peter Atuya mmewe Mwakilishi wa Wadi ya Bokeira, Kaunti ya Nyamira Callen Atuya katika eneo la Tombe eneo bunge la Kitutu Masaba, Naibu gavana huyo alisema yeyote aendaye kwenye mazishi anafaa kuomboleza wala sio kupiga siasa pahala pa huzuni.
"Nawaambia viongonzi na wanasiasa kuwa wakati huu ni kuwatumika wananchi kimaendeleo bali sio siasa ya kila mara haswa wakati wengine wanaomboleza. Siasa kwenye mazishi ni aibu kubwa,” alisema Nyaribo, naibu gavana Kaunti ya Nyamira.
Nyaribo aliongeza, "Tunapohudhuria mazishi kuomboleza tukiingiza siasa wanafamilia waliofiwa watasema sio kuomboleza tulikujia ila kupiga domo ya siasa. Hebu tujiheshimu kama viongonzi kwa kukoma tabia hiyo."
Pia naibu huyo alisema Serikali ya kaunti hiyo ipo imara kufanya maendeleo kwa wananchi wote wa kaunti hiyo huku akiwomba viongonzi walio katika mamlaka katika kaunti hiyo kushirikiana pamoja ili kupeleka maendeleo kwa wakaazi hao.
“Tulichaguliwa kuwa viongonzi ili tufanye maendeleo, mbona tusitimize ahadi tulizowaahidi waliotupa kazi? Nawaomba tuungane tutafute suluhu halisi ya shida zinazowakumba wakaazi wa eneo hili ili tuimarishe maisha yao kimaendeleo,” alidokeza Nyaribo.
Viongonzi waliohudhuria sherehe hiyo ya mazishi miongoni mwao ni Mbunge wa Mugirango Kaskazini Charles Geni, Spika wa Kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko, Mbunge wa bunge ya Afrika Mashariki Joseph Kiangoi na Wawakilishi wa Wadi mbali mbali.