Katibu Mkuu wa chama cha ODM Ababu Namwamba, ameahidi kuwaunganisha viongozi wa chama kutoka kaunti ya Nyamira ambao kwa mwaka sasa hawashirikiani na gavana wa kaunti John Nyagarama.
Akiongea siku ya Ijumaa kwenye mji wa Nyamira kwenye kampeni ya kuwahimiza wakazi kujiandikisha kupata vitambulisho, kampeni ambayo cha ODM kimekuwa kikiendeleza tangu siku ya Alhamisi, Namwamba alisema viongozi kutoka kaunti ya Nyamira sharti washikane ili kuwa mfano kwa wananchi ambao wanawaongoza.
Bw Namwamba aliwahakikishia wakazi kutoka kaunti hiyo kuwa atamwalika kiongozi wa Cord Raila Odinga aje kutafuta suluhu miongoni mwa viongozi wa kisiasa ambao alisema huenda wataleta utengano kwenye chama hicho na kuwataka wawe na umoja ili ikifika uchaguzi ujao, chama hicho kiweze kuchukua mamlaka.
Miongoni mwa viongozi ambao wamekuwa na mzozo baina yao na gavana Nyagarama ni mwakilishi wa wanawake Bi Alice Chae, Mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire, Mbunge wa Mogirango Magharibi Dr James Gesami na mbunge wa eneo bunge la Mugirango Kaskazini Charles Geni.
Viongozi hao wameshtumiwa na wakazi kwenye kaunti kwa kutumiwa na vyama pinzani kuvuruga uongozi wa kaunti hiyo ya Nyamira.
Mwakilishi wa wadi wa Bonyamatuta ambaye alikuwa na wenzake kwenye mkutano huo aliwataka viongozi wakuu wa chama hicho wakiongozwa na Raila Odinga kutafuta mwafaka na kuwaleta viongozi hao pamoja kabla ya mambo hayajaenda kombo kwenye chama hicho tawi la Nyamira.