Share news tips with us here at Hivisasa

Katibu Mkuu wa chama cha ODM Ababu Namwamba ameikosoa serikali ya Jubilee kwa kumwondoa Naibu Inspekta wa Polisi Grace Kaindi ofisini.

Kulingana na katibu huyo, serikali inastahili kufuta katiba ya Kenya ambayo inaeleza bayana kuwa kunapaswa kuwa na usawa wa jinsia katika nyadhifa za uongozi nchini.

Alikuwa akizungumza siku ya Ijumaa  katika eneo la Itare eneo bunge la Bomachoge Borabu kaunti ya Kisii.

Namwamba alizuru kaunti ya Kisii kuwahimiza wananchi hasa vijana kujiandikisha na kuchukua vitambulisho na kadi za kupiga kura kwa wingi ili kupata fursa ya kuchagua viongozi wanaotaka ifikapo mwaka wa 2017.

Namwamba aliikosoa serikali na kusema Grace Kaindi hakuwa na makosa yoyote ambayo yangesababisha kuondolewa kutoka wadhifa wake.

“Grace Kaindi hakuwa na makosa ya kuondolewa afisini na hiyo ni ishara ya kuonyesha kuwa serikali ya Jubilee imeshindwa na kazi hapa nchini,” alisema Namwamba.

Pia, alipinga hatua ya kuteuliwa kwa mwanamme kuchukua wadhifa wa Bi Kaindi akisema ikiwa serikali ilihitaji kufanya mabadiliko katika sekta ya usalama, basi wadhifa huo ungechukuliwa na mwanamke.

Bw Namwamba alitangaza wazi kuwa yeye kama katibu mkuu katika chama cha ODM hawezi kuunga mkono baadhi ya sekta ambazo ziko chini ya uongozi wa kaunti kurudishwa kwa serikali kuu na kusema kuna haja ya kuongeza pesa kwa kaunti bali si kurudisha sekta katika serikali ya kitaifa kutoka kwa kaunti.