Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama ameanzisha mashirika ya waendeshaji bodaboda katika kila sehemu ya kaunti ili kuwanufaisha wahudumu hao.
Mashrika hayo yatawasaidia waendeshaji bodaboda kuwa katika vikundi na kujipatia mikopo ambayo itawasaidia kufanya biashara na kujiendeleza kimaisha.
Mikopo hiyo ambayo wahudumu hao watakuwa wakipokezwa ni ya serikali ya kaunti hiyo.
Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo la Ekerenyo wakati mashirika hayo yalianzishwa, Gavana Nyagarama alisema mashirika hayo yameanzishwa ili waendeshaji bodaboda hao wayatumia kujinufaisha wao wenyewe.
“Mashirika haya yatawasaidia vijana wetu hapa kwa kaunti haswa wale wa umri mdogo na waendeshaji bodaboda ili waweze kujinufaisha wenyewe,” alisema Nyagarama.
Waendeshaji bodaboda ambao walihudhuria hafla hiyo ya ufunguzi wa mashirika hayo katika eneo la Ekerenyo walimpongeza Gavana Nyagarama kwa kusema kuwa hiyo ni mojawapo ya njia ya kuwakumbuka na kuwasaidia kukuza biashara zao na kujiinua kukimaisha.
“Sisi kama waendeshaji bodaboda tunashukuru gavana kwa kuanzisha mashirika haya katika kaunti yetu ya Nyamira na tutafaidika maana ukijiandikisha kwa kikundi, itakuwa rahisi kukabidhiwa mkopo na kuanza biashara,” alisema peter Ongeri mwendeshaji bodaboda.
Wakazi nao walisema vijana hao wa umri mdogo watafaidika pakubwa na kuwaomba vijana hao pindi watakapoanza kupewa mikopo hiyo kutoka kwa mashirika hayo, wahakikishe wanafanya jambo ambalo litakuwa kama kumbukumbu kwa maishani yao yote.