Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama ametia sahihi na shirika moja lisilo la kiserikali kutoka nchi ya Merekani kwa jina Global Ped kuimarisha sekta ya afya Nyamira.
Hii ni baada ya shirika hilo kukabidhi serikali ya kaunti hiyo mashine ya kupima magonjwa mbalimbali kama njia moja ya kuimarisha sekta ya afya katika kaunti ya Nyamira.
Akizungumza mnamo siku ya Alhamisi katika ofisi ya gavana mjini Nyamira wakati wa makubaliano hayo ya kutia sahihi, mwenyekiti wa shirika hilo Monwel Kolnel alisema makubaliano ya kutia sahii na serikali ya Nyamira ni ishara ya kuimarisha sekta ya afya katika kaunti hiyo ili watu wapate huduma ya matibabu kikamilifu.
Kwa upande wake, Gavana Nyagarama alisema mashine hiyo ya kupima magonjwa mengi zaidi mwilini itasaidia kupima watu kutoka kaunti zote bali siyo wa kutoka Kaunti ya Nyamira tu.
“Nalishukuru shirika hili kwa kutusaidia na mashine itakayotumika kupima magonjwa katika hospitali ya Nyamira Level Five na kusaidia kujua mgonjwa mbalimbali ya anayepimwa kabla ya kutibiwa,” alisema Nyagarama.
Ikimbukwe kuwa Kaunti ya Nyamira ndio ilikuwa ya kwanza kuwa na mashine ya CT scan pamoja na ile ya Mobile clinic na kaunti hiyo imeahidi, kupitia Gavana Nyagarama, kuwa itahakikisha watu wanapata huduma bora ya mtibabu ili sekta ya afya imarike katika kaunti hiyo.
“Nahitaji sekta ya afya iongoze kwa huduma bora maana watu sharti wawe na afya nzuri na mengine kufuata,” aliongeza Nyagarama.