Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ameombwa kujitokeza wazi na kuelezea jinsi pesa za kukarabati barabara zimetumiwa na Serikali ya kaunti hiyo.

Akiongea jana katika eneo la Chitago ilioko eneo Bunge la Mugirango Kusini, Mbunge wa eneo hilo Manson Nyamweya alimtaka Gavana Ongwae kuelezea jinsi pesa za kukarabati barabara zilizoko katika kanti hiyo zimetumiwa na serikali yake huku akidai kuwa hamna maendeleo yamefanyika haswa katika upande wa barabra za kaunti ya Kisii.

“Gavana Ongwae anastahili kutuambia ameweka lami barabara ya kutoka eneo fulani kuelekea eneo lingine lakini sio kutuambia kuwa amekarabati barabara kwa kuweka mchanga.Mbona kaunti zingine kama Machakos, Wajir na Meru barabara zao zimewekwa lami?,” aliuliza Mbunge Nyamweya.

“Tukiwa na barabara za lami katika Kaunti ya Kisii hatutakuwa na changamoto kama kusumbuliwa na matope na magari kukwama matopeni,” alisema Nyamweya.

Aidha mbunge huyo alisema serikali za ugatuzi zilianzishwa nchini ili kufanya maendeleo katika sehemu za mashinani haswa kwa kuzikarabati barabara na kuwekwa lami ili wananchi waone matunda ya serikali za ugatuzi.

Hii sio mara ya kwanza mbunge huyo kuonekana kuwa na tofauti kwa maendeleo ya Gavana Ongwae kwa kumkosoa na ikumbukwe kuwa mbunge huyo ana nia ya kuwania kiti cha ugavana ifikapo mwaka wa 2017.

Mbunge Nyamweya alitangaza kuwa na nia hiyo mapema mwaka huu kuwa atakiwania kiti hicho cha ugavana ili kuwafanyia maendeleo wakaazi wa Kaunti ya Kisii.