Naibu Gavana wa Kaunti ya Nyamira Amos Nyaribo ametofautiana na hatua ya Gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama kutaka kuwarejesha kazi mawaziri wanne na makatibu wawili waliosimamishwa kazi kwa tuhuma za ufisadi miezi miwili iliyopita.
Akirejelea taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti moja la humu nchini kuhusiana na madai kwamba huenda Gavana Nyagarama akalazimika kuwarejesha kazini mawaziri na makatibu hao kufuatia hatua ya wawakilishi wa bunge la kaunti hiyo kutupilia mbali ripoti ya kamati iliyoteuliwa kuwachunguza dhidi ya tuhuma za ufisadi, Nyaribo amekana kuambiwa na Gavana Nyagarama iwapo taarifa hiyo ni ya ukweli.
"Iwapo taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti moja la humu nchini kuhusiana na kurejeshwa kazini kwa maafisa husika, kwangu mimi naweza sema kuwa Gavana Nyagarama hajanihusisha kuhusiana na swala hilo,” alisema Nyaribo.
Akizungumza siku ya Jumatano, Nyaribo alisema kwamba huenda Gavana Nyagarama alinukuliwa visivyo na kuongezea kuwa sharti mashauriano yafanywe kabla ya hatua kama hiyo kutekelezwa.
"Nafikiri kuwa huenda ripota aliyeandika taarifa hiyo alimnukuu Gavana Nyagarama visivyo na iwapo hatua kama hiyo yafaa kuchukiliwa, sharti kuwe na mashauriano,” alisema Nyaribo.