Share news tips with us here at Hivisasa

Mgomo wa walimu unapoingia wiki ya tatu, walimu kutoka Kaunti ya Mombasa wamemtaka mkurugenzi wa tume ya kuwaajiri walimu nchini Dkt Lidiah Nzomo kukoma kuwapa walimu vitisho vya kuwafuta kazi.

Walimu hao walisema kuwa watandelea kupigania haki yao hadi dakika ya mwisho na kusisitiza kuwa watarudi madarasani wakati hela zao zitakapoingia kwenye akaunti zao za benki.

Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Mombasa, katibu mkuu wa chama cha Knut tawi la Kilindini, Bwana Dan Oloo, alisema ni kinyume na sheria walimu kupewa barua na hata viongozi wao kutishiwa ilhali walimu hao wanapigani kile ambacho mahamaka makuu yaliamua.

Oloo alisema kuwa ni haki yao kugoma kama inavyosema katika katiba ya Kenya.

Aliwashauri walimu wote pamoja na viongozi wa vyama vya Knut pamoja na Kuppet kukaza kamba na wasiweke roho mkononi.

Alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kufanya hima na kuwaita viongozi husika ili kutafuta suluhu la kulipwa kwa walimu hela za nyongeza ya mishahara yao.

“Ualimu ni taaluma ya heshima na sharti ipewe staha inayostahili. Si haki walimu kunyanyaswa kila mwaka na kupewa ahadi za uongo kila wakati. Sharti walimu walipwe hela zao ili nao waishi kama wafanyakazi wengine kwenye idara zingine za serikali,” alisema Oloo

Aliongezea, “Zile pesa ambazo zinaendelea kutumiwa vibaya na idara zingine zitumiwe kuwalipa walimu.”