Share news tips with us here at Hivisasa

Wahalifu mjini Nakuru wameonywa na kutahadharishwa kuwa siku zao zimehesabika.

Akizungumza afisini mwake siku ya Ijumaa, OCPD wa Nakuru Bernard Kioko alisema kwamba visa vya uhalifu mjini Nakuru vimepungua kwa kiwango kikubwa kutokana na kupunguza msongamano katika mji huo.

Isitoshe, Kioko alisema kwamba hata ruhusu wakazi pamoja na wageni wanaozuru mji huo kuporwa bidhaa zao kinyume na ilivyokuwa hapo mbeleni.

“Awali ilikuwa vigumu mno kwa maafisa wa polisi kukabiliana na wahalifu kutokana na msongamano mjini,” alisema Kioko.

Mkuu huyo wa polisi aliwaonya wahalifu dhidi ya kuwaibia watu mali yao mjini Nakuru, hususan wezi wa mifuko.

Kioko ambaye pia ni kasisi amewataka wahalifu wote waache mienendo hiyo miovu, na badala yake waokoke.

Ingawa kioko hakutaja ni mbinu gani anazotumia pamoja na zile atakazotumia ili kuwanasa wahalifu pamoja na wezi hao, alisema kuwa tayari mbinu hizo zimeendelea kuzaa matunda.