Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae ameanzisha mradi wa kusafisha mji wa Nyamache ulioko eneo bunge la Bobasi ili kuimarisha mazingira ya eneo hilo.
Gavana alianzisha mradi huo siku ya Alhamisi alipotembelea eneo hilo la Nyamache ili kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ongwae pia alianzisha mradi wa upasuaji katika hospitali ya Nyamache level four ili watu wawe wanapata huduma ya upasuaji katika hospitali hiyo.
Mradi huo wa usafi utakuwa ukitekelezwa na vijana wa huduma kwa taifa (National Youth Service) katika eneo hilo.
Gavana Ongwae alisema kuwa sekta ya mazingira inatarajiwa kuinuliwa zaidi katika kaunti ya Kisii ili wananchi wawe wakifurahia mazingira mema ambayo hayatadhuru afya yao.
Mradi wa kusafisha miji mbambali katika kaunti hiyo ya Kisii umekuwa ukifanywa na vijana wa huduma hiyo ya ambao waliajiriwa hivi majuzi.
Mradi huo ulianzia mji wa Kisii na kuendelea kutekelezwa hadi sehemu mbalimbali za kaunti hiyo.
Ongwae aliwaomba wananchi kuendelea kutunza mazingira kwani mazingira mema huleta afya nzuri kwa wananchi.
“Kila mwananchi anastahili kuwajibika kwa kutunza mazingira na kufanya usafi ili watu wasije wakaathirika kiafya,” alisema Gavana Ongwae.
Wakazi walifurahishwa na mradi huo wa kusafisha miji ambao wengi walisema unapaswa kupewa kipao mbele.