Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae amesema kuwa yeye kama kiongozi hatakubali sekta ya afya kusimamiwa na serikali ya kitaifa tena.
Akizungumza siku ya Ijumaa katika hospitali ya rufaa na mafunzo iliyoko mjini Kisii, Ongwae alisema mabadiliko yameonekana tangu serikali za ugatunzi zianze kusimamia sekta hiyo.
“Tangu sekta ya afya iwe nchini ya uongonzi wa serikali za ugatunzi, huduma za matibabu zimebadilika haswa katika hospitali ya Rufaa ya Kisii. Nimeweka mashine za 'CT scan', 'Dialisis', pamoja na ile ya 'Digital Diagnosis'. Hatutakubali sekta ya afya kuregeshwa chini ya mamlaka ya serikali ya kitaifa,” alisema Gavana Ongwae.
Aliongeza: “Tunahitaji sekta ya afya ibaki chini ya uongonzi wa serikali za ugatuzi ili huduma hiyo ya matibabu iendelee kama ilivyokuwa imeanza tangu tuingie mamlakani kama magavana.”
Matamshi ya Gavana Ongwae yaliungwa mkono na wakaazi wa kaunti hiyo ambao walisema wao kama wakazi hawawezi kubali sekta hiyo kurudishwa chini ya uongozi wa serikali ya taifa.
“Tangu sekta ya afya isimamiwe na serikali za ugatuzi huduma ya afya imeimarika zaidi," alisema Christopher Mbaka, mkazi.
“Mabadiliko ambayo tumeshuhudia ni makubwa hasa tangu sekta hiyo ya afya iwekwe chini ya uongozi wa serikali ya kaunti. Mie napendekeza kila sekta iwekwe chini ya uongozi wa kaunti,” alisema Victor Mose, mkazi.