Chifu wa lokesheni ya Mochenwa wadi ya Gesima, amepewa majina ya wagema wote katika eneo hilo ili aweze kuwachukulia hatua ya kisheria.
Akiongea siku ya Alhamisi katika ofisi yake ilioko eneo bunge la Kitutu Masaba, Kaunti ya Nyamira wakati wakupokea majina hayo kutoka kwa wakazi, Chifu Magara Makori alisema kuwa orodha hiyo itawasaidia kukabiliana na wagema hao.
Chifu Magara alisema kuwa walichukua hatua hiyo ya kuandika orodha ya wagema kwa kila kijiji ili kuweka mikakati ya kukabiliana nao.
Aidha, chifu huyo aliwaonya wote walioko katika orodha hiyo na kusema kuwa hatua na kisheria itachukuliwa dhidi yao.
“Nitahakikisha kuwa yeyote aliye katika orodha hii kama mgema amechukuliwa hatua kali ya kisheria kwa kuwa tumekuwa tukifanya msako na wengine wanachukulia kuwa ni mchezo wa paka na panya,” alisema chifu Magara.
Majina zaidi ya wagema 100 yalitolewa kwa ushirikiano wa wananchi na wazee wa vijiji kama njia moja ya kumaliza pombe haramu katika lokesheni hiyo.
Kwingineko, wakazi wa lokesheni hiyo wameombwa kusaidia maafisa wa polisi wa utawala kutoka kituo cha Gesima katika uchunguzi wa kumsaka mwanamume mmoja anayedaiwa kuwatishia wazee wakijiji alipopatikana na pombe haramu nyumbani kwake katika kijiji cha Nyabiosi.
Kwa sasa maafisa wa polisi wanamtafuta mwanamume huyo na wamemuomba mtu yoyote aliye na habari kuripoti katika kituo cha polisi cha Gesima.