Share news tips with us here at Hivisasa

Huku wakazi wakutoka kaunti ya Kisii wakijihusisha na aina mbalimbali za kilimo, ukosefu wa pesa umetajwa kuwa kikwazo kikuu kwa wakulima hao kuweza kuanzisha kilimo cha uyoga.

Kilimo hicho cha ambacho kinaendelezwa na kutekelezwa kwa kutumia teknolojia ya hali juu, miongoni mwa mahitaji ambayo huwataka wakulima kujenga nyumba spesheli za kukuza aina hiyo ya mboga pia imechangia wengi kujitoa na kutojihusisha na kilimo hicho.

Kwenye mahajiano na mkurugenzi mkuu wa kilimo katika kaunti ya Kisii Bwana Nathan Soire, wakulima wengi kutoka kaunti hiyo hawana uwezo wa kifedha wa kuwaruhusu kuweza kuanzisha kilimo cha Uyoga, kilimo ambacho alitaja kuwa kina mapato sana iwapo wakulima wangejiunga hata kwa makundi ili waweze kuendeleza kilimo hicho.

Bwana Soire alisema kuwa wameweka juhudi za kuhakikisha wanawaelimisha wakulima jinsi wanaweza kupata mikopo kutoka kwenye taasisi ya kifedha ili kujiendeleza, na kuwataka kufanya kilimo kama taaluma yoyote ile ambayo watu wengine hufanya na kuwaletea pesa, hivyo kwa kufanya kilimo kama biashara itawapa hela ambayo watatumia kufanyia shughuli nyingi za kilimo.

Mbali na changamoto hiyo ya kifedha miongoni mwa wakulima, mkurugenzi huyo wa kilimo pia alisema kuwa wakazi wengi walikuwa wamezoea kula uyoga wa kukua msituni ambao wanapata bure bila malipo, hali ambayo alisema imekuwa mazoea kwa wakazi wa Kisii kwani inakuwa vigumu kwao kununua uyoga kwa vile hawajazoea.

Aliwashauri wakulima na wakazi kwa jumla kutoka kaunti hiyo kuacha kuwa na mienendo ya kuzoea kupata bidhaa bure, bali wajaribu kuwafaa wakulima wanaoinukia kwa kununua bidhaa zao ili nao wapate hela ya kuendeleza kilimo chao.