Idara ya usalama katika ukanda wa Pwani imewatahadharisha vijana waliojitosa katika uhalifu kujinasua katika magenge hayo na kusitisha kuenea kwa visa vya kihalifu kwani maafisa wa usalama wanawaandama.
Akitoa kauli hiyo mjini Mombasa siku ya Jumanne, Kamanda mkuu wa Polisi eneo la Pwani Francis Wanjohi alisema kwamba vijana wengi wa umri mdogo wamejiunga na makundi ya kihalifu na kusababisha hofu miongoni mwa wakazi kwa kisingizio cha ukosefu wa ajira.
Wanjohi aliwaonya vijana hao kujitenga na magenge hayo na kuzisaidia jamii zao katika maswala ya kujikimu maishani, kwani idara ya usalama kamwe haitaruhusu mtu yeyote kuwahangaisha wakazi wasiokuwa na hatia.
“Tunawaonya vijana waliyojiunga na makundi ya kihalifu kujisalimisha kabla ya maafisa wa polisi kuwaandama kwani serikali itaruhusu mtu yeyote kuwahangaisha wakazi wasiokuwa na hatia,” alisema Wanjohi.
Aidha, amewataka wakazi kushirikiana kwa karibu na maafisa wa usalama katika kutoa habari kuhusu washukiwa wa uhalifu ili wakabiliwe na maafisa wa usalama kikamilifu na eneo hilo kuwa salama.
Kauli ya Kamanda huyo imejiri siku chache tu baada ya afisa mmoja wa polisi kupigwa risasi na kufariki papo hapo na genge la majambazi waliyofanikiwa kutoroka na bunduki ya afisa huyo.