Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa polisi wilayani Nyamira, kaunti ya Nyamira wameanzisha uchunguzi wa kuwasaka washukiwa wa mauaji  ya mwanamke mmoja wilayani humo.

Hii ni baada ya mwili wa mwanamke mmoja wa umri wa makamo kupatikana umetupwa  katika mto wa Charachani siku ya Jumatatu asbuhi wilayani Nyamira.

Kulingana na mkuu wa polisi wilayani Nyamira Ricah Ongare, aliyezungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu asubuhi, mwanamke huyo anashukiwa kuuliwa katika sehemu tofauti na mwili wake kuletwa na kutupwa katika mto huo.

“Maafisa wa polisi wameanzisha uchungunzi wa kuwatia mbaroni waliohusika na mauaji hayo, lakini huenda mwanamke huyu aliuliwa katika sehemu tofauti kisha mwili wake ukashafirishwa na kutupwa katika mto huu wa charachani,” alisema Ongare.

Mwili wa mwanamke huyo ulisafirishwa hadi chumba cha kuhifadhi maiti cha Nyamira.

Kwa upande wa wakazi, wamehofia maisha yao kufuatia mauaji hayo, huku wakiomba maafisa wa polisi kuimarisha usalama kila wakati ili kupunguza visa vya mauaji hayo katika kaunti ya Nyamira.

“Tunaomba maafisa wa polisi kuweka usalama wa kutosha katika kila sehemu ya kaunti ya Nyamira kwani kitendo hiki si kitendo cha kwanza katika eneo hili, watu ni wengi ambao wamepatikana wameuawa katika mto huu wa Charachani,” alisema Marion Mokeira, mmoja wa wakaazi.