Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baadhi ya waliokuwa maafisa wa polisi na wengine ambao wanahudumu kwa sasa wanashirikiana na wahalifu kuiba vyuma vya shirika la reli katika eneo la Nakuru.

Haya yamesemwa na afisa mkuu wa polisi wa Nakuru Railways Justiva Nzito, aliyezungumza na wanahabari Ijumaa.

Afisa huyo aameashiria kuwa tangu mwezi Machi mwaka huu, wamenasa angalau lori sita zilizokuwa zikisafirisha vyuma kuelekea katika maeneo ya Londiani, Bahati, Solai na maeneo mengine.

Hata hivyo, amebainisha kwamba baada ya uchunguzi, ilionekana kuwa matukio yote yameshirikishwa na baadhi ya waliokuwa maafisa wa polisi na wengine ambao wanahudumu kama maafisa wa polisi kwa sasa kwa njia ya moja kwa moja au kwa njia nyinginezo.

"Nataka kuhimiza umma kutujuza kuhusiana na wale ambao wanahusika katika uhalifu wa wizi wa vyuma, ambao umeongezeka pakubwa mjini Nakuru. Tunataka kuwaonya waliokuwa maafisa wa polisi wanaohusika katika hatia hii," alikariri Nzito.

Kulingana naye, Lori moja lilinaswa hivi maajuzi likisafirisha vyuma vyenye thamani ya shilingi milioni 1.7 katika eneo la Solai, lakini cha kushangaza ni kwamba kulikuwa na maafisa watatu wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Solai waliokuwa wamelipa ulinzi.

Hata hivyo, amefichua kuwa maafisa hao watatu walitoweka baada ya kugundua kuwa walikuwa wakifuatwa.

"Nilipata maafisa wa polisi wakisindikiza lori hilo lakini walipotuona walitoroka lakini tulifanikiwa kujua wanakohudumu na baada ya hayo nilimwarifu mkuu wangu kuhusiana na hilo. Maafisahao wanahusika kikamilifu katika tukio hilo na inakadiriwa kuwa thamani ya vyuma hivyo ilikuwa shilingi milioni 1.7," aliashiria Nzito.

Wakati huo huo, Nzito amesema vyuma vya reli vilivyoibiwa vinapelekwa katika soko la vyuma Mjini Kisumu na katika mji wa Eldoret.

Aidha, afisa huyo amehimiza umma kujitokeza kutoa habari mhimu kuhusiana na hilo kwa maafisa wa polisi.