Chama cha kutetea haki za kibinadamu katika Kaunti ya Kisii, kimewakosoa maafisa wa polisi kwa kuchelewa kuwatia mbaroni wawakilishi wa wadi waliofunga ofisi mbili za serikali katika kaunti hiyo wiki moja iliyopita.
Wawakilishi hao walifunga ofisi inayosimamia fedha na ile ya karani kwa madai ya kutolipwa pesa za marupurupu ya vikao.
Akizungumza siku ya Jumatatu na waandishi wa habari katika mji wa Kisii baada ya kutoka katika ofisi ya mkuu wa polisi wilayani Kisii ya kati Francis Nguri kulalamikia kitendo hicho, mwenyekiti wa chama hicho, Vincent Gekonge, aliwakosoa maafisa wa polisi kwa kutowatia mbaroni wawakilishi hao hadi sasa.
Gekonge alisema wameshangazwa sana kwa kuwa hata mshukiwa mmoja hajatiwa mbaroni na ushahidi ungalipo.
Alisema kuwa kazi ya wawakilishi ni kufanya maendeleo bali si kuharibu bidhaa vya ofisi kwa kulalamikia kutolipwa marupurupu ya vikao ambavyo hawakuvihudhuria.
“Leo tulikuja kwa ofisi ya mkuu wa polisi kujua kwa nini wawakilishi hao bado hawajatiwa mbaroni hadi sasa, ilhali waliharibu bidhaa, mali na kufunga ofisi mbili za serikali. Tunahitaji haki itendeke,” alisema Gekonge.
Aliongeza: “Kama chama, tunataka wawakilishi hao watiwe mbaroni na wachakuliwe hatua za kisheria kwa kukosa nidhamu.”
Mkuu wa polisi wilayani Kisii ya Kati Francis Nguri alisema uchunguzi unaendelea hadi sasa na pindi utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa
“Uchunguzi unaendelea ili tutambue wale walioshambulia ofisi na kutekeleza uhalifu. Tutawajulisha ni akina nani na hatua itachukuliwa dhidi yao,” alisema Nguri.