Share news tips with us here at Hivisasa

Hakimu mkuu wa mahakama ya Nakuru amewaonya maafisa wa polisi dhidi ya kuwazuilia watuhumiwa wa uhalifu gerezani kwa zaidi ya saa ishirini na nne kabla hawajafikishwa kortini.

Akizungumza siku ya Jumatano, hakimu mkuu wa Nakuru Doreen Mulekyo alisema makosa ya kucheleweshwa kwa wafungwa kufika kizimbani kujitetea yamekithiri na yanahitaji kuchunguzwa.

Mulekyo alisihi kiongozi wa chama cha wanasheria (LSK) tawi la Nakuru David Mongeri, kuwashtaki maafisa wa usalama wanaowazuilia watuhumiwa korokoroni zaidi ya saa ishirini na nne kwani ni kinyume cna sheria na wanakiuka haki za mshtakiwa.

Alisisitiza kuwa upande wa mashtaka unafaa kubadilisha mbinu za utekelezaji wa majukumu yao ili wawezeshe idara ya mahakama kutoa haki kwa washukiwa.

Aliongeza kuwa iwapo maafisa wanaohusika na tendo hilo watachukuliwa hatua za kisheria, watakuwa funzo kwa wenzao.

"Upande wa mashtaka unapaswa kubadili njia wanazotumia kutekeleza majukumu yao ili mahakama itoe haki kwa washtakiwa. LSK inafaa kuwafungulia mashtaka maafisa wanaohusika ili wawe mfano mwema kwa wenzao," alisema Mulekyo.