Share news tips with us here at Hivisasa

Idara ya polisi katika eneo la Likoni imewataka wakazi kutoa habari kwa maafisa wa polisi kusuhu vijana wanaodaiwa kupotea na kupokea mafunzo ya kigaidi nchini Somalia.

Akizungumza katika afisi za CDF huko Likoni siku ya Jumanne, Afisa mkuu wa polisi katika eneo hilo Willy Simba alisema kwamba maafisa wa polisi mara nyingi huusishwa na tuhumu za kupotea kwa vijana hao.

Simba amepinga madai ya kuhusika kwa maafisa wa polisi na tuhuma hizo, na akasema kwamba hatua ya kutoa habari muhimu kwa maafisa wa polisi kuhusu walikotoweka vijana hao kutasaidia pakubwa kuwatafuta.

“Maafisa wa polisi hawawezi kuhusika na kupotea kwa vijana, sisi ndio tunalinda wananchi na lazima tuhakikishe wananchi wako salama. Ikiwa kuna mtu ana habari zozote kuhusu kule vijana hao waliko, basi tujulishwe na tutafuatilia mara moja,” alisema Simba.

Afisa huyo wa polisi amewashinikiza wazazi kuwashauri vijana wao jinsi ya kujiepusha na maswala ya uhalifu na misimamo mikali, na kujihusisha na maswala ya maendeleo katika jamii ili kuimarisha usalama.

“Wazazi wana jukumu kubwa la kuwashauri vijana wao kule nyumbani kwani hao ndio wanatambua vyema mienendo ya vijana. Wazazi ikiwa watafanya hivyo, basi tutaweza kuzuia vijana wengi kwenda kule nchini Somalia kujiunga na Alshabab,” aliongea afisa huyo.

Wakati huo huo, Simba aliwataka wakazi wa eneo hilo kuendelea na mpango wa nyumba kumi, huku akisema kwamba usalama kupitia kwa mpango huo umeimarishwa kwa kiasi kikubwa.