Share news tips with us here at Hivisasa

Baraza la wazee wa jamii ya Agikuyu limehimiza idara ya polisi kuchunguza na kubaini kinachopelekea makahaba kuuawa mjini Nakuru.

Baraza hilo kupitia kwa msemaji wake Gilbert Kabage limetaka maafisa hao wa polisi kuwakamata wanaotekeleza uovu huo na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Kabage aliyekuwa akizungumza siku ya Alhamisi mjini Nakuru, alisema kuwa wao pia ni binadamu walio na haki, sawia na ilivyo kwenye katiba ya Kenya na kutokana na hilo, wanafaa kulindwa kwa njia yoyote ile.

“Tuna vitengo mbalimbali kama vile vya ujasusi, upelelezi na polisi. Kwahivyo, tungependa wafanye uchunguzi kwa sababu ni vibaya kwa watu kuuawa ovyoovyo na hata ingawa wao wanafanya kazi hiyo, wao pia ni binadamu. Hakuna mtu ambaye ana haki ya kuua mwingine,” alisema Kabage.

Matamshi yake yanajiri baada ya kahaba mmoja kuuawa mjini Nakuru siku ya Jumamosi, wiki iliyopita.

Aidha, tukio hilo lilijiri baada ya makahaba wengine wawili kuuawa katika muda wa mwezi mmoja.