Kiwango cha pombe haramu katika kaunti ya Kisii kimekuwa chanzo kikubwa cha maafa na mizozo ya kinyumbani miongoni mwa familia.
Haya yalisemwa siku ya Jumapili, mshirikishi wa shirika la kupigana na matumizi ya dawa za kulevya na unywaji pombe haramu, NACADA, eneo la Nyanza Askofu Laurence Nyaanga, alisikitikia kiwango cha wanaume kwa wanawake ambao wameathirika na unywaji pombe kwenye viunga vya Kisii ambako aliwataka machifu na manaibu wao kukaza kamba ili kung’oa uraibu huo katika jamii zetu.
Askofu huyo ambaye alikuwa katika operesheni ya kunasa wenye vibanda vya kutengeneza pombe katika mji wa Kegati, alionya vijana kuwa huenda kusiwe na kizazi katika maisha ya baadaye iwapo wataendelea kujitia katika unywaji pombe ambayo huwekwa sumu ambayo hudhuru afya.
Msako huo unafanywa baada ya mtu mmoja kudaiwa kunywa pombe na kuaga dunia katika mji wa Birongo ambapo alipatikana siku moja tu baada ya maafisa wa polsi kutoka kituo kimoja katika eneo hilo kuonekana kupiga doria katika nyumba za kuuza pombe na kusemekana kupewa hongo wakaachilia wanywaji pamoja na wale wanaouza pombe hiyo.
Katika opereshini hiyo zaidi ya lita elfu 15, ziliweza kumwagwa katika eneo hilo na baadhi ya wapikajia na wauzaji wa vileo hivyo kukamatwa ambapo watashitakiwa dhidi ya kuuza na kutengeneza pombe haramu.
Mshirikishi huyo aliapa kupigana dhidi ya watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya pamoja na pombe haramu katika eneo zima la Nyanza hadi dakika ya mwisho ambapo kufika jana ilikuwa wiki ya pili baada ya kuanzisha operesheni hiyo kwa ushirikianao na utawala wa mkoa.