Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mamlaka ya kudhibiti Pareto nchini, PRA, imefanikiwa kulipa deni la wakulima ililokuwa inadaiwa kwa miaka kadhaa.

Hii ni baada ya serikali ya kitaifa na serikali ya kaunti ya Nakuru kuingilia kati na kuwapa fedha za kufufua kilimo hicho.

Kufikia tarehe nne mwezi wa Septemba, PRA ambayo ilijulikana kama Bodi ya Pareto ya Kenya, PBK, ilikuwa imewalipa wakulima hadi ya mwezi wa Juni. Kwa sasa PRA inajitayarisha kuwapa malipo ya mwezi wa Julai na Agosti.

Kulingana na meneja mkuu anayesimamia maswala ya nyanjani kaunti ya Nakuru, Mary Ontiri, kilimo cha pareto ambacho kilianzia 1928 nchini, kimeanza kunawiri tena katika kaunti 18 nchini, huku wakipokea kiwango kikubwa cha Pareto kutoka kaunti ya Pokot.

"Serikali kuu inatutengea shilingi milioni 300 kila mwaka, na fedha hizo zinatusaidia kumaliza madeni tuliyokuwa nayo ya wakulima,” alisema.

Charles Kariuki kutoka wizara ya kilimo ya Nakuru, amesema kuwa serikali ya kaunti ya Nakuru inajikakamua kuongeza mbegu za pareto kila mwaka, ili wakulima wafaidike zaidi.

“Mwaka huu wa kifedha tumechagua wakulima fulani watakaokuza mbegu hizo. Kiasi cha ardhi ambapo pareto inakuzwa kimeongezeka. Mwaka wa 2013 ilikuwa hektari 447, na kwa sasa tumefika zaidi ya hektari 900," Kariuki aliongeza.

Ontiri alisema kwa sasa wanalipa mkulima kwa kati ya shilingi 100 hadi 325 kwa kilo moja kulingana na ubora wa pareto ya mkulima, ikiwa mkulima amezingatia ushauri.

Kiwanda cha pareto kilicho Nakuru ndicho kikubwa zaidi nchini, na kina uwezo wa kusaga kilo milioni 20 za pareto kwa mwaka mmoja.