Kiongozi wa muungano wa upinzani Raila Odinga amewataka viongozi wote wa kisiasa kutoka eneo la pwani kupinga mswada wa ardhi kwa dhati, akisema kuwa nia ya mswada huo ni kuleta mgongano kati ya jamii zote nchini hasa wakazi kutoka eno la pwani ambao mara nyingi wamekuwa na mizozo inayohusiana na ardhi.
Alisema kuwa iwapo mswada huo utapitishwa na ardhi ya jamii kurejeshwa katika mikono ya serikali kuu kupitia katika wizara ya ardhi, kuna uwezekano wa kuleta mzozo hasa katika zile kaunti ambazo zimekuwa zikidhulumiwa na serikali za awali katika masuala ya mashamba eneo la pwani likiwa katika nafasi ya mbele.
Akiongea sku ya jana Jumamosi katika hoteli moja mjini Mombasa katika kongamano la magavana wa kaunti sita pwani lililoitwa Jumuiya ya Kaunti za Pwani, kiongozi huyo wa upinzani aliwataka viongozi wa pwani pamoja na viongozi wengine walio na nia njema kusimama kidede na kupinga mswada.
“Sisi kama ODM na CORD tutapinga mswada huo kwa hali na mali, na nawaomba viongozi wote wa upinzani msimame na msimamo mmoja kwa sababu mswada huu unaturudisha nyuma,” alisema kiongozi huyo wa upinzani.
Kwa upande wake gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Joho, ambaye alihudhuria kwenye mkutano, aliwataka wabunge wa upinzani na wabunge wengine walio na azimio la kuendeleza maendeleo nchini kuupinga mswada huo.