Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Rais Uhuru Kenyatta ameombwa kuingilia kati swala la mishahara ya walimu.

Rais ameombwa kuagiza tume ya kuajiri walimu nchini 'Teachers service commission' (TSC) kulipa walimu kulingana na agizo la mahakama.

Wito huo umetolewa baada ya ishara kuonekana kuwa tume ya kuwajiri walimu nchini TSC na wizara ya elimu haijaitikia agizo la mahakama hadi sasa.

Akizungumza siku ya Jumatano mjini Gucha, mwenyekiti wa chama cha KNUT wilayani Gucha, Samwel Nyairo alisema hawatakubali kuwa na mazungumzo yoyote na serikali bila kuongezwa mshahara jinsi ilivyoagizwa na mahakama kuu nchini.

Nyairo aliomba Rais Kenyatta kuingilia kati na kuagiza tume hiyo ya TSC na Wizara ya elimu kuweka pesa kwa akaunti za walimu kabla ya Agosti 31, 2015 ili walimu kupata haki yao.

Pia aliomba wazazi kutopeleka watoto wao shuleni wakati shule zitakapofungiliwa mwezi ujao ikiwa hawatapewa mishahara yao mwisho wa mwezi huu.

“Tulishinda tume ya TSC mahakamani na lile limesalia ni kuwekewa pesa zetu kwa akaunti. Naomba Rais Uhuru asinyamaze na ajitokeze wazi na kuagiza tupatiwe pesa zetu kwani ni haki yetu,” alisema Nyairo.