Hatimaye wanafunzi wa shule ya Mayatima ya Vision of Hope katika eneo la Jomvu kaunti ya Mombasa walioathirika na funza sasa wamepata matibabu maalum kutoka kwa shirika la kijamii la ‘Miritini Jamii Rescue Team’.
Akiongea na wanahabari baada ya zoezi la kuwapa matibabu wanafunzi hao katika eneo Jomvi mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Mwenyekiti wa Shirika hilo Halima Ali alisema kwamba kutokana na ukosefu wa mazingira safi katika maeneo ya makazi kumechangia kuenea kwa maradhi ya kiafya ikiwemo funza kwa jamii.
Kulingana na Halima, eneo la Jomvu limeathirika pakubwa na funza, na akahoji kwamba kuna haja kwa maafisa wa sekta ya afya kuzuru katika maeneo hayo na kutibu maeneo ya wakazi ili kuwaepusha na maradhi mbalimbali ya kiafya na jamii kuishi katika mazingira safi.
“Kuna haja ya maafisa wa sekta ya afya kuzuru mashinani na kuyatibu mazingira ya wakaazi ili kuwaepusha na maradhi mbalimbali ya kifya, ikiwemo funza kwani hali inayoikumba jamii na watoto huenda ikawaletea madhara zaidi,” alisema Halima.
Halima alielezea kusikitishwa na wakazi wa maeneo hayo jinsi walivyoathiri na funza hao huku wazee wakishindwa hata kutembea kutokana na vidole vyao kushambuliwa na wadudu hao na kuwasababishia afya duni.
“Ni jambo la kusitisha watoto wadogo na wazee wakiathirika na maradhi ya funza huku maafisa wa afya wakisalia katika afisi badala ya kuzuru mashinani na kuwaokoa kizazi cha kesho. Lazima kuwepo na ushirikiano ili kuwasaidia ndugu zetu,” aliongeza Halima.
Amehoji kuwa shirika hilo linalenga kuzuru mashinani na kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira safi sambamba na kuwalinda watoto wao kutokana na kukumbwa na maradhi mbalimbali ya kiafya.