Wadau katika sekta ya hoteli mjini Eldoret wamesema idadi ya hoteli za kifahari mjini humo inazidi kuongezeka.
Wadau hao walisema kuwa idadi hiyo inatokana na kuwepo kwa mazingira bora ya uwekezaji katika sekta hiyo.
Kwa mujibu wa muungano wa wamiliiki hoteli mjini humo, vitanda katika hoteli za mji huo vimefikia kiwango cha 3,000.
Akizungumza siku ya Ijumaa mjini Eldoret, Mshrikishi wa wamiliki hao Bw Joseph Wainaina alisema kuwa idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2018.
“Kwa sasa hoteli zetu zina vitanda zaidi ya 3,000. Hii ni mojawapo ya matunda ya ugatuzi,” alisema Wainaina.
Bw Wainaina alitaka serikali ya kaunti ya Uasin Gishu kuendelea kuboresha miundo msingi katika kaunti hasa barabara ili kuvutia wawekezaji zaidi.
Wainaina alitaka serikali ya kitaifa kushirikiana na wadau katika sekta hiyo kuboresha usalama mjini humo.
Kiongozi huyo alitaka idara ya usalama kutafuta mbinu ya kuhakikisha kuwa kila hoteli ya kifahari ambayo iko viungani mwa mji huo imepewa askari waliojihami.
“Serikali inapaswa kutupatia askari waliojihami kwa bunduki ili kuhakikishia wateja wetu usalama wao,” aliongeza Wainaina.
Bw Wainaina alitaka wamiliki hoteli husika kuhakikisha kuwa wanalipa ushuru unaohitajika ili kuwezesha serikali kutoa huduma inayostahili kwa Wakenya wote.