Seneta wa Kaunti ya Uasin Gishu Isaac Melly anatarajiwa kufika kwenye mahakama moja ya Nakuru mwezi ujao, kujibu shtaka la kuongoza maandamano yaliyosababisha wanafunzi wa Chuo kikuu cha Eldoret kuharibu mali.
Uamuzi huo umetolewa baada ya seneta huyo kukosa kufika mahakamani siku ya Alhamisi kwa kuwa alikuwa nje ya nchi.
Kutokana na hilo, upande wa mashtaka umetaka Seneta Melly aagizwe afike mahakamani mara moja pindu tu atakapowasili nchini.
Hakimu mkuu Nyakundi Maroro aliagiza kesi hiyo iendelee tarehe Novemba 12, 2015.
Melly pamoja na washtakiwa wengine wawili wanadaiwa kuongoza maandamano katika chuo kikuu hicho yaliyopelekea mali kuharibiwa siku ya Februari 12, 2015.
Inadaiwa wanafunzi wa chuo hicho kikuu waliandamana huku wakitaka naibu chansela wao Profesa Teresia Akeng’a atimuliwe.
Mwezi Oktoba mwaka huu, Chuo kikuu cha Eldoret kilimshtaki Melly mahakamani kikitaka kufidiwa kwa uharibifu wa mali uliosababishwa na maandamano hayo.