Seneta wa Kaunti ya Nyamira Kennedy Okong'o ametoa ilani ya siku 14 kwa tume ya kuwaajiri walimu humu nchini (TSC) kuwalipa walimu mshahara wao wa mwezi wa Septemba ilivyoamuriwa na mahakama.
Akiongea mjini Nyamira siku ya Jumatatu, Senator Okong’o ambaye pia ni mwananchama wa Kamati ya Elimu ya Seneti, alisema kuwa tume hiyo ya TSC inastahili kuwalipa walimu mishahara yao ama wachukuliwa hatua za kisheria.
“Mahakama ilikuwa imetoa uamuzi kuwa walimu walipwe mshahara wao wa mwezi wa Septemba na hadi sasa sielewi kwa nini tume ya TSC haijatimiza uamuzi huo. Nitafika mahakamani kuishtaki TSC kwa kukiuka uamuzi wa mahakama,” alisema Okong’o.
Okong’o alisema kuwa atahakikisha kuwa maafisa wakuu wa TSC wamefika mbele ya Kamati ya Elimu ya Seneti kuelezea sababu ya kutowalipa walimu.
“Kamati ya Elimu ya Seneti inatayarisha kukutana na mwenyekiti wa TSC Lydia Nzomo ili aweze kutumbia sababu ya kutowalipa walimu. Na ikiwa tume hiyo haitakuwa imewalipa walimu baada ya muda wa siku 14 sijazo, nitaishtaki,” aliongezea Okong’o.