Serikali ya Kaunti ya Kisii itachimba Kisima katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Nyamache kama njia moja ya kuleta suluhu kwa shida ya maji katika eneo hilo.
Akiongea siku ya Jumapili katika shule hiyo ya Nyamache wakati wa hafla ya mchango, Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae aliwahakikishia wakazi kuwa serikali yake itachimba kisima katika shule hiyo ili kumaliza shida ya maji ya kuwasaidia wakazi wa eneo hilo.
“Hii ni moja miongoni mwa miradi ambayo serikali ya Kaunti ya Kisii imeipa nafasi ya kwanza kwa kuwa maji ni uhai na kila mwananchi anahitaji maji katika shughuli zake za kila siku,” alihoji Gavana Ongwae.
Aidha, alisema mikakati kabambe imewekwa ya kutoa maji kutoka mito ilioko karibu na mahali hapo ili kila mkazi aweze kuyapata nyumbani mwake.
“Ni ombi langu kuwa wakati serikali ya kaunti itatoa pesa za kujenga bomba la maji wale watakaopewa kandarasi hiyo wawe wanatengeneza kwa ukamilifu kwani mara nyingi wengi huyatengeneza mabomba hayo kisha baada ya wiki moja yanaharibika na kuleta shida ya ukosefu wa maji,” alidokeza Sibia Mong’ina, mkazi.