Huenda uchukuzi wa bidhaa za shambani pamoja na usafiri kwa jumla kurahisishwa, baada ya serikali kitaifa kudokeza kuwa ujenzi wa barabara kuu kutoka Kisii, Ahero hadi Isabania utaanza kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Akiongea siku ya Ijumaa na wanahabari katika taasisi ya mafunzo ya uhandisi ya Kenya Institute of Highway and Building Technology katika hafla ya kufuzu kwa wanafunzi, mhandisi Phelemon Kilimo kutoka wizara ya Barabara na Utunzi wa Miundomsingi alisema kuwa tayari wasoroveya wametumwa kuanza kufanya utafiti na utathmini wa barabara hiyo ambayo huunganisha kaunti tatu za Nyanza Kusini.
Kilimo aliwahakikishia wakazi kuwa sasa itakuwa rahisi kwa kaunti husika kuweza kuboresha usafirishaji wa mazao ya shambani, na iyo itakuwa barabara ya kwanza kubwa katika eneo la Nyanza kusini, na kudokeza kuwa serikali kuu itaendelea kukarabati barabara nyingine ambazo zinasimamiwa na serikali ya kitaifa.
Aidha, aliwashauri vijana kutoka kaunti za Nyamira kuanza kujisajili kwenye masomo ya uhandisi katika taasisi hiyo ili kusaidia kulainisha upungufu ulioko wa waandisi wa barabara kote nchini.
Kilimo pia alishauri serikali ya kaunti ya Kisii kuwasilisha orodha ya barabara ambazo zina viwango vya kilomita kati ya sita na tisa ili kufanyiwa utathmini na wizara ya barabara na kama zinastahili kukarabatiwa na KURA au KERRA.