Serikali kuu imezidi kulaumiwa kwa kutowahusisha wadau mbalimbali pamoja na viongozi wa kaunti ya Mombasa katika kulitatua tatizo la msongamano wa abiria katika kivuko cha feri cha Likoni mjini Mombasa.
Kulingana na Naibu Gavana wa kaunti ya Mombasa Hazel Katana, tatizo la kushuhudiwa kwa misongamno ya mara kwa mara katika kivuko hicho ni usimamizi duni uliyochangiwa na serikali kuu kutowahusisha wadau mbalimbali na viongozi wa kaunti ya Mombasa.
Akiongea na wanahabari baada ya kushuhudiwa taharuki katika kivuko hicho eneo la Likoni mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Katana alisema kwamba wasimamizi wa Shirika la huduma za feri wanapaswa kuchunguzwa na kueleza bayana tatizo kuu linaloikumba shirika hilo ili litatuliwe na feri hizo kuwafaidi wakenya.
“Tunastaajabishwa na serikali kuu jinsi inavyolishughulikia tatizo la feri katika kivuko cha Likoni. Tuliwaambia tukae pamoja na tusemezane ili tulitatue kwa pamoja tatizo hili na kupunguza msongamano wa mara kwa mara, lakini serikali kuu imeonekana kukwepa swala hilo,” alisema Katana.
Naibu huyo aidha alisema kwamba tangu serikali za kaunti zigatuliwe, serikali kuu ilidinda kutenga shirika la huduma za feri kusimamiwa na serikali ya kaunti ya Mombasa na kuchangia hali ngumu ya wakazi wanatumia kivuko hicho cha feri ya Likoni.
Haya yamejiri baada ya feri ya MV Kwale kukumbwa na hitalafu za kimitambo na kusababisha msongamano mkubwa wa abiria katika kivuko hicho na zaidi ya wakazi 15 wakijeruhiwa walipokuwa wakisukumana wakati wa kuabiri feri asubuhi ya leo.