Kila nyumba katika kaunti ya Nyamira inatarajiwa kupokea neti moja kwa kila watu wawili kufuatia mikakati iliyowekwa na serikali ya kaunti hiyo kwa ushirikiano na shirika la afya duniani kuhakikisha kuwa wananchi wanapewa neti.
Akiongea afisini mwake, katibu wa wizara ya afya kwenye serikali ya kaunti ya Nyamira Dkt Douglas Bosire alisema kuwa shughuli hiyo ya usambazaji neti itasaidia pakubwa kupambana na ugonjwa wa malaria, hasa msimu huu wa mvua.
"Tayari tumepokea neti elfu 500,00 na kila nyumba ya watu wawili itapokea neti mbili, na kwa sababu ya msimu huu wa mvua ya El-nino serikali yetu kwa ushirikiano na shirika la afya duniani tumeamua kuchukua hatua za mapema kuthibiti malaria,” alisema Bosire.
Bosire aidha aliwasihi wananchi waliojisajili kupokea neti hizo kujitokeza kwa wingi kwenye kambi za chifu na manaibu wao pamoja na zahanati mbalimbali ili kupokea neti hizo, huku akiongezea kuwa machifu pamoja na polisi wa utawala watatumiwa kwenye shughuli hiyo.
"Sasa ni jukumu la wananchi kujitokeza kwanzia siku ya Alhamisi kulingana na vile tutakavyo watangazia ili kuchukua neti zao na shughuli hiyo itaendeshwa kwenye kambi za machifu na manaibu wao pamoja na zahanati zitakazo teuliwa na maafisa wa polisi wa utawala watasaidia kwenye shughuli hiyo," alisema Bosire.
Bosire amechukua fursa hiyo kuwaonya maafisa wowote watakaotumia wakati huu kuwahadaa wananchi kuwa neti hizo ni za kuuzwa ilhali zinapeanwa bila malipo.