Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Nyamira imeweka mpango wa kuimarisha huduma za matibabu katika Hospitali Kuu ya Nyansiongo wilayani Borabu.

Akizungumza siku ya Jumatatu, afisa mkuu wa afya katika kaunti ya Nyamira Douglas Bosire, alisema kuna uhaba wa vyumba vya kulala vya wagonjwa katika hospitali hiyo.

Bosire alisema kuwa wameweka mpango wa kukamilisha ujenzi wa ghorofa kwenye hospitali hiyo, itakayo tumika kama vyumba vya wagonjwa.

"Ujenzi wa ghorofa hiyo utakapokamilika kutakuwa na vyumba vya kutosha kwa wagonjwa. Ni matumaini yangu kuwa huduma hiyo itaimarishwa vilivyo,” alisema Bosire.

Aidha, Bosire alisema kuwa ili kufanikisha mpango huo, serikali ya kaunti itashirikiana na wadau wengine ili kumaliza ujenzi wa ghorofa hiyo.

"Kwa hivi sasa tumepanga mchango siku ya Ijumaa wiki hii kwenye hospitali hiyo ya Nyansiongo ili kuchanga pesa za mradi huo kwa ushirikiano na wadau mbalimbali," alisema Bosire.